Aya
25
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT AL-INSHIQAAQ
(Imeteremka Makka)
Sura hii imetaja baadhi ya ishara za Saa ya Kiyama, na kunyenyekea ardhi na mbingu kufuata atakavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na imefahamisha kwamba mtu anachungwa ende akakutane na Mola wake Mlezi, na kwamba vitendo vyake vimeandikwa katika daftari atakalo kuja likuta. Basi mwenye kulipokea kwa mkono wake wa kulia, hisabu yake itakuwa nyepesi. Na mwenye kulipokea kwa mkono wa kushoto atayayatika kuipata adhabu na kuingia Motoni. Tena Mwenyezi Mungu Subhanahu ameapa kwa Ishara ambazo zinashuhudia uweza wake, na ambazo zinaitia imani ya kufufuliwa. Lakini juu ya hayo walio kufuru hawaamini, wala hawaizingati Qur'ani, wala hawazifuati hukumu zake. Kisha Sura inakhitimisha kwa kuonya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayo dhamiria, na kwamba Yeye amekwisha waandalia adhabu iliyo chungu, kama alivyo waandalia Waumini ujira wa daima usio katika.