Makka
Sura Ta Ha

Aya

135

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT T'AHA 

(Imeterenka Makka)

SURA hii ni ya Makka, isipo kuwa Aya mbili, nazo ni Aya 130 na 131, Hisabu ya Aya zake ni 135. Sura hii imeanza kwa harufi mbili za kuzindua juu ya muujiza wa Qur'ani na kuwazindua wasikilizaji waisikilize. Baada ya harufi hizo mbili cheo cha Qur'ani kimetaijwa, na utukufu wa hii Qur'ani ni utukufu wa Mwenye kuileta, naye ni Mwenyez Mungu, Subhanahu wa Taa'la, Mmiliki mbingu na ardhi, Mwenye kujua siri, na kilicho fichikana kuliko siri. Kisha kimesimuliwa kisa cha Musa (AS) pamoja na Firauni, na vip alipo anza kupewa utume Nabii Musa (AS) Na yametajwa maombi yake kutaka nduguye Harun (AS) awe msaidizi wake wa kumpa nguvu, tena vipi walivyo kutana na Firauni baada ya kitisho cha mkutano wake kwa ajili ya ujeuri wake. Na katika mintarafu ya haya Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha kuzuka kwa Musa (AS).

Katika Sura hii pana majibizano baina ya Musa na Firauni, tena baina ya Musa (AS) na wachawi. na hali ya Musa ya kuogopa kushindwa mbele ya wachawi, na fimbo yake ilipo zimeza kamba zao, na tena mwisho vipi yalivyo ishia mambo ya wachawi na kuamini kwao, na Firauni kuwaadhibu. Kisha ikatajwa vipi Musa alivyo toka yeye na Wana wa Israili kutokana na Firauni, na vipi alivyo zama Firauni, naye alikuwa kawafuatia baada ya kupasuka bahari: na vipi Musa aliokoka akafika Jabal Tur akawaacha watu wake ili ende kwenye mlima kuzungumza na Mola wake Mlezi. Na Msamaria akawafitini kwa kuwachochea waliabudu sanamu la ndama lililo undwa kwa dhahabu. Na ilikuwa ukipita upepo ndani yake hutoa sauti. Musa alikasirika kwa yaliyo tokea, akamkamata kichwa nduguye akimvutia kwake.

Kisha katika Sura hii tukufu akatokea yaliyo msibu Msamaria. Mwenyezi Mungu Subhanahu amesimulia hadithi ya kuvuka katika hadithi za Musa na nyenginezo. Na mwisho wa Sura pana mausio mema juu ya Subira, na Usamehevu, na Sala. Kisha ikabainishwa kubwatika washirikina katika matakwa yao ya muujiza mwengine usio huu wa Qur'ani; na Subhanahu ameashiria hikima ya kuwatuma Mitume. Tena Sura hii tukufu imekhitimisha kwa kuashiria adhabu watakayo pata makafiri, na malipo mema watakayo pata Waumini.