Aya:
206
Mahali iliteremshwa:
Makka
Ali Muhsin Al-Barwani - Swahili Translation of Al-Muntakhab
SURAT AL- A'RAAF
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeteremka Makka isipo kuwa Aya nane, nazo ni 163 mpaka 170. Na idadi za Aya zake ni 206.
Mwanzo wa Sura hii ni kuendeleza yaliyo kuja mwisho wa Sura ya Al-Ana'm, na baada ya hayo imeingia kueleza khulka ya kibinaadamu. Ikataja kisa cha Adam na Hawa. na walivyo toka kwenye Bustani kwa kutiwa wasiwasi na Shetani, na ikaeleza huo wasiwasi unaoendelea kwa watu katika mAyazi na chakula. Kisha Aya za Sura hi tukufu, kama sura nyengine za Qur'ani zikaingia kutupia jicho kwenye mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, na kuzingatia uumbaji wake wa ajabu.
Kadhaalika Sura hii imeeleza hadithi za Manabii kama Nuhu na Hud na kaumu yake kina A'ad Kisha hadithi ya Saleh na kaumu yake, Thamud, walio sifika kwa nguvu zao na wakapewa utajiri; na hadithi ya Lut na kaumu yake, na ikataja maovu waliyo kuwa wakiyafanya; na hadithi ya Shua'ib na watu wa Madyana. Na baada ya hadithi hizo za kweli Sura imeeleza mafunzo na mazingatio yaliyomo: Naye Subhanahu wa Ta'ala amefuatilizia hayo kwa kisa cha Musa na yaliyo tokea katika mambo ya Firauni.
Na Sura ikakhitimishia kwa kumathilisha nini hali ya mwenye kupewa hidaya khalafu akabanduka kwenye uwongofu akaingia kwenye upotovu kwa kumfwata Shetani, na Sura pia ikamalizia kueleza Wito wa kuendea Haki alio kuja nao Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.