Aya
11
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT AL MUNAFIQUUN
(Imeteremka Madina)
Sura hii imekusanya kikundi cha sifa za wanaafiki; ikataja kwamba hao hutangaza imani yao kwa ndimi zao bila ya kuwa wanasema kweli. Na ikabainisha kwamba wanafanya yamini zao za uwongo kuwa ni kinga wasiambiwe kuwa ni makafiri, ambao kwa hakika ndivyo walivyo na ndivyo watakavyo lipwa hivyo. Pia imebainisha kuwa wana umbo zuri la kumpendeza anao waona, na wana ufasihi mzuri kusikilizwa.Na juu ya hivyo, nyoyo zao zi tupu, hazina Imani ndani yake. Wao ni kama magogo yaliyo egemezwa, yasiyo na uhai.
Na Sura inaelezea kuwa wakiitwa ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghfira, hali yao hubainika kwa kuwa hutakabari, na hudhihirisha kukataa kwao kuitikia, nao wanajivuna.
Kisha Sura ikaingia kutaja madai ya wanaafiki kwamba wao ati ndio watukufu wenye nguvu, na Waumini ni madhalili; na ahadi walio waahidi Waumini kuwa watawatoa mji wakisha rejea Madina. Sura imebainisha wepi katika makundi mawili hayo walio watukufu na wenye nguvu.
Na khatimaye Sura inaelekeza kuwasemeza Waumini watoe kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, wafanye haraka kwa hayo kabla mauti hayajamfikia mmoja wao. akajuta, na akatamani laiti inge akhirishwa ajali yake. Na wala Mwenyezi Mungu hamuakhirishi yeyote ikisha fika ajali yake.