Aya
200
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT AL I'MRAN
(Imeteremka Madina)
MIONGONI mwa mambo inayo yazungumzia Qur'ani ni hadithi za ada ya Mwenyezi Mungu katika uumbaii wake, na mifano na mazingatio yanayo patikana katika hizo hadithi. Na hubainisha katika hadithi hizo mambo mengi yaliyo khusu itikadi, hukumu za sharia na nyendo njema. Katika Sura iliyo pita yametajwa mfano wa mwendo wa Wana wa Israili. Yameelezwa mengi ya walivyo kengeuka. Na katika Sura hii yanatajwa mengine ya upotovu wao na kukengeuka kwao, na vipi Muumini anatakikana aongoke katika itikadi yake na mwenendo wake, na pia unabainishwa humu ukweli wa Dini ya Mbinguni, na inaonyeshwa vipi ziwe adabu za kujadiliana, na zinaelezwa ada za wakati wa kushinda na pengine wakati wa kushindwa. Pia inabainishwa vipi watakuwa wanao kufa Mashahidi Siku ya Kiyama, na yepi malipo yao. Na hayo yote kwa wanaume na wanawake. Na inaelezwa kadhaalika njia ya mafanikio. Sura hii tukufu inaanza kama ilivyo anza iliyo tangulia.