Aya
45
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT QAAF
(Imeteremka Makka)
Mwanzo wake Sura hii inasimulia kuthibiti Utume wa Muhammad s.a.w. na wanavyo kanya makafiri kuja Mtume kati yao, na kuona muhali kufufuliwa baada ya kwisha geuka dongo. Na ikaeleza Ishara za uumbaii zinazo onyesha dalili ya kwamba Mwenyezi Mungu hashindwi kuwafufua watu baada ya kufa kwao, na hali Yeye ndiye aliye waumba hapo kwanza, na anajua yanayo wapitikia katika nafsi zao.
Na Yeye anavisajili vitendo vyao na maneno yao katika Daftari lenye kuhifadhi hata dogo. Na Sura imebainisha kwamba majaribio ya makafiri Siku ya Kiyama kutaka kuukataa ukafiri walio kuwa nao duniani, ati kwa kusingizia walikuwa ni wafwasi tu wa Mashetani hayatawaletea nafuu yoyote. Kwani mwisho wa mjadala wao ni kutumbukizwa wote katika Moto, na huku Mwenyezi Mungu anawafadhili Waumini kwa kuwapa neema za milele katika Pepo. Kisha Sura inamalizikia masimulizi yake kwa kumuamrisha Mtume s.a.w. avumilie maudhi ya makafiri ambao hawakuzingatia yaliyo wapata walio kadhibisha katika kaumu zilizo kuwa kabla yao, na kumwelekeza Mtume s.a.w. athibiti juu ya ibada ya Mwenyezi Mungu, na kutilia mkazo hili jambo la kufufuliwa, na kumliwaza Mtume s.a.w. kwa kuwa yeye ni mwenye kuwakumbusha Waumini, wala si mtawala wa makafiri.