Madina
Sura Al-Jumua

Aya

11

Mahali iliteremshwa

Madina

SURAT AL-JUMUA 

(Imeteremka Madina)

Imefunguka Sura hii kwa kutoa khabari yake Mtukufu kwamba viliomo katika mbingu na ardhi vyote vinamsabihi Yeye. Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka shani yake amesema kwamba ameineemesha kaumu isio jua kuandika wala kusoma kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao, ambaye anawafundisha Kitabu, na hikima, na anawatakasa. Na hakika hii ni fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewakemea Mayahudi kwa kuacha kwao kutenda yaliyo amrishwa katika Taurati, na hali wao wanajua yaliomo humo. Na amepinga madai yao kwamba wao peke yao ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu, si watu wenginewe. Na amebariziana nao kwa kuwataka watamani kufa ikiwa wao wanasema kweli! Na Sura imekhitimisha kwa kuwaamrisha Waumini wakimbilie kwenda sali Sala ya Ijumaa pindi wakisikia adhana, na waache biashara. Na Sala ikisha malizika watawanyike katika nchi wende kutafuta fadhila za Mwenyezi Mungu. Na kawakataza wasiache biashara au jambo la pumbao lolote kuwashughulisha wasiisikilize khutba ya Ijumaa. Na Mwenyezi Mungu amewadhamini kuwaruzuku, na Yeye ndiye mbora we kuruzuku.