Aya:
29
Mahali iliteremshwa:
Madina
SURAT AL-H'ADIID
(Imeteremka Madina)
Sura hii imeanzia kwa kueleza kwamba wote walioko mbinguni na katika ardhi wamemsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kika kisicho kuwa laiki naye. Kisha ikafuatiliza hayo kwa kuelekeana na kusabihi huko ufalme wa mbingu na ardhi, na kuvizunguka vyote hivyo na kuviendesha. Kisha Sura ikaamrisha Imani ya Mwenyezi Mungu, na kutoa katika njia yake, na ikabainisha khitilafu za daraja za kutoa kwa mujibu wa kukhtalifiana haja ziliopo na dharura zake. Kisha ikaeleza sura ya Waumini Siku ya Kiyama, inavyo tangulia nuru yao mbele yao na pembezoni mwao: na sura ya wanafiki wanavyo waomba Waumini wawangojee ili nao wapate mwangaza kutokana na nuru yao. Na baina yao umesimamishwa ukuta wenye mlango. Ndani yake ipo rehema, na nje yake upande wa mbele yake ni adhabu.
Na Sura ikaingia baada ya hayo kuwahimiza Waumini wanyenyekee kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na Haki aliyo iteremsha. Na inawaonyesha vyeo vya wanao sadiki wanaume na wanawake mbele ya Mola wao Mlezi; na mwisho wa Makafiri wanao kadhibisha ni katika Jahannamu. Na inapiga mifano ya udhalili wa dunia na hizo starehe zake, na ukubwa wa Akhera na neema na adhabu zilioko huko.
Na Sura inataka watu wawanie kushindania maghfira kwa Mwenyezi Mungu, na inazituza nafsi kwamba kila kinacho msibu mtu ikiwa kheri au shari kimeandikwa katika Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu, ili nyoyo zinyenyekee kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu. Kisha ikasimulia khabari za kuwatuma Mitume na kuwafuatiliza mmoja baada ya mmoja wakipewa nguvu kwa hoja na Vitabu, na njia za nguvu na vitendo, ili watu wasimamishe uadilifu.
Kisha Aya ikakhitimisha kwa kuwaita Waumini wamche Mungu, na ikawaahidi kuwa watapewa rehema maradufu na watafanyiwa hisani ya kufadhiliwa, ambayo hapana mwenye kuiweza hata kidogo ila Mwenyezi Mungu. Kwani hakika fadhila zote zimo katika mkono wa Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.