Makka
Sura Al-Muumin

Aya

85

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT GHAAFIR (AU AL MUUMIN) 

(Imeteremka Makka)

Sura hii imeanzia, kama zilivyo anzia Sura nyingi, kwa harufi mbili katika harufi za Alifbete. Na ikaanza kwa kutaja shani ya Qur'ani iliyo teremka kutokana na Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi, Mwenye kusamehe madhambi, Mwenye kukubali toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu. Kisha ikaitia Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, na kuacha kudanganyika na utawala ambao huenda makafiiri wakawa nao, na ikawataka watu wakumbuke matokeo ya kaumu zilizo kuwa kabla yao. 

 Baada ya hayo Sura imesimulia khabari za wabebaji A'rshi, na kusabihi kwao, na madua yao. Na ikaeleza hali ya makafiri, na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu juu yao. Na Sura ikasimulia zaidi kuliko mara moja juu "ya Ishara za Mwenyezi Mungu na uwezo wake katika nafsi zao, na yaliyo wazunguka ya mbinguni na kwenye ardhi, na neema zinazo wamiminikia, kama inavyo waitia katika zaidi kuliko Aya moja  wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kwa kumuabudu Yeye tu: "Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu." Na alisema Mola wenu Mlezi: “Niombeni, nitakuitikieni!" "Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi Mungu, Muumba wa kila kitu. Hapana mungu isipo kuwa Yeye." 

Kama vile vile Sura hii ilivyo kusanya katika baadhi ya Aya zake maneno ya kukumbusha Siku ya Mwisho: "Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni nao wamejaa huzuni.” Na Sura imesimulia kidogo katika kisa cha Musa (AS) pamoja na Firauni, na khasa walio amini katika watu wa Firauni. 

Na Sura ikakhitimishia kwa kuwataka watu watembee katika ardhi waone yaliyo wafika kaumu zilizo kuwako kabla yao, na vipi ulikuwa mwisho wa ghururi zao kwa ilimu walizo kuwa nazo. Na ilipo wafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu walisema: Tunamuamini Mwenyezi Mungu pekee, na tunawakanya hao miungu tuliyo kuwa tukimshirikisha nao. Lakini hao wameamini baada ya kwisha pita wakati, "Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa wakati ambao wamekwisha iona adhabu yetu." Na huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake, wala hutakuta mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu. Na inapo shuka adhabu hapo ndipo watapo khasiri makafiri.