Aya
54
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT FUSS'ILAT (AU H'A MIM SAJDAH)
(Imeteremka Makka)
Sura hii imeanzia kwa harufi mbili katika harufi za alifbete kama inavyo fanya Qur’ani katika Sura nyingi. Sura hii imeeleza katika nyingi ya Aya zake shani ya Qur'ani na mambo iliyo kusanya yaliyo khusu bishara na maonyo. Na imeeleza msimamo wa washirikina kukhusu Qur'ani, katika kuipuuza na kuupiga vita wito wake, na msimamo wa Mtume kwa mnasaba wa makafiri, kwa kusimama imara juu ya wito wake kwao na kuwaambia. "Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi tengeneeni kumwendea Yeyena mumtake msamaha."
Na Sura inaingilia kuwakumbusha washirikina uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuziumba mbingu na ardhi kisha inawahadharisha na yaliyo watokelea watu wa mataifa walio karibu mno na makwao, nao ni kina A'adi na Thamudi. Na inawakumbusha Siku ya Akhera, siku yatakapo washuhudia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao, kwa waliyo kuwa wakiyatenda; na mijadiliano itakayo kuwa baina yao na viungo vyao siku hiyo; na watayo yaomba wafwasi kwa Mola wao Mlezi Siku ya Kiyama: "Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe wale walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa." Na kama ilivyo kuwa mwendo wa Mwenyezi Mungu katika Kitabu hichi akisimulia khabari ya makafiri, husimulia pia khabari za Waumini. Basi Sura hii imesimulia khabari za walio sema: "Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu", kisha wakasimama sawa sawa, neema za daima alizo waneemesha, na akalinganisha baina ya kheri na shari: "Wema haulingani na uovu".
Kisha Sura inataka watu waangalie Ishara za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu zinazo onyesha kumkinika kufufuliwa maiti, kisha inarejea tena kuzidi kuwakemea wanao zigeuza Aya za Mwenyezi Mungu, na kwamba hao hawamkhofu Mwenyez Mungu. Na kwamba hakika Kitabu hichi hakiingiliwi na upotovu kutoka mbele yake wala nyuma yake. Huu ni mteremsho ulio tokana na Mwenye hikima, Msifika. Na hakika Ujumbe wa Muhammad si ujumbe ulio zuliwa tu.
Na Sura inathibitisha khulka moja katika khulka za binaadammu, nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu akimneemesha mtu huipuuza Haki, na ikimgusa tu shari anakuwa na madua marefu marefu.
Na Sura imekhitimisha kwa kuthibitisha mambo mawili muhimu kabisa, nayo ni la kwanza: kutaja kwa Qur'ani Tukufu yenyewe Haki iliyomo ndani yake isiyo na shaka yoyote: "Tutawaonyesha Aya zetu katika upeo wa macho na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli." Na la pili lake kuwa hilo wanalo litegemea makafiri Si lolote ila ni shaka tu ya kufufuliwa iliyo wapelekea kuwa nayo ukafiri na upotovu. "Ama hakika wao bado wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi, Hakika Yeye amekizunguka kila kitu."