Sura Al-Qamar

Aya

55

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT AL-QAMAR 

(Imeteremka Makka)

Imekuja Aya ya kwanza katika Sura hi kuzindua kuwa watu wasikilize kwamba kiyama kinakaribia, na watu wanahadharishwa na tukio hilo. Kisha zimekuja Aye nyengine baada yake kuweka wazi msimamo wa makafiri kwa mintarafu ya miujiza na kushikilia kwao kukadhibisha. Na anatakiwa Mtume s.a.w. awapuuze na awangojee mpaka siku watakapo toka makaburini kama nzige walio tapanyika. 

Tena baada ya hapo Aya zikawa zinafuatana, zikieleza hali namna mbali mbali za mataifa yaliyo tangulia kwa mnasaba na Mitume wao, na adhabu iliyo washukia. Na baina ya kila kisa na kingine inazindua mawazo ya kwamba Qur'ani tukufu imefanywa nyepesi kwa mwenye kutaka kuwaidhika na kuzingatia.

Mwishoe inabainisha kwamba hao makafiri wa Makka si watu wenye nguvu zaidi au wakali zaidi kushinda mataifa yaliyo kwisha tangulia, na kwamba wao si wenye kuiepuka adhabu. Tena Sura ikakhitimisha kwa kuwahadharisha wanao kadhibisha wenye inda kuwa mwisho wao watakuja tumbukizwa Motoni kifudifudi, na wataambiwa: Onjeni mguso wa Jahannamu mliyo kuwa mkikadhibisha. Na inawatuza wachamngu katika maskani zao za Mabustanini na mito, katika makao mazuri kwa Mfalme Mwenye uweza.