Makka
Sura Al-Jathiyah

Aya

37

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT AL-JAATHIYA 

(Imeteremka Makka)

Imeanzia Sura hii kwa harufi mbili katika harufi za Alifbete, na kubainisha kuwa kuteremshwa Qur'ani kumetokana na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu Mwenye hikima. Kisha ikazitaja dalili za uumbaji na za kiakili kuthibitisha itikadi ya Imani na kuitia watu waifuate. Hali kadhaalika imekusanya wito kwa wenye kukadhibisha Ishara. Kisha ikaingia kuzihisabu neema za Mwenyezi Mungu na fadhila zake kwa waja wake; na ikawataka Waumini wawasamehe makafiri wanao kanya Kwani Mwenyezi Mungu peke yake ndiye wa kumlipa kila mtu kwa alilo litenda.

Kisha Sura baada ya hayo ikazungumzia vipi Mwenyezi Mungu alivyo wafadhili Wana Israili kwa kuwapa neema nyingi, na khitilafu zilizo zuka baina yao ambazo Mwenyezi Mungu atazitolea hukumu Siku ya Kiyama. Kisha ikaingia kufarikisha baina ya walio fuata Haki na walio fuata matamanio, wakakanya kufufuliwa, na wakapinga Ishara za uweza kwa kutaka wafufuliwe baba zao! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuhuisha, na ndiye Mwenye kufisha. Yeye ana ufalme wa kila kitu. Na siku watakapo kusanywa wapotovu kila nafsi itaitwa ikapokee kitabu chake. Hapo watafuzu Waumini na watakemewa walio takabari. 

Sura tena inarejea hadithi ya kule kuikataa kwao Saa ya Kiyama, na kuzikadhibisha Ishara zinazo ionyesha; na vile Mwenyezi Mungu atavyo wasahau wao kama wao walivyo isahau hii Siku. Na ikabainisha kuwa makaazi yao ni Motoni kwa kule kuzikejeli kwao Ishara za Mwenyezi Mungu na kudanganyika kwao na dunia. Na Sura imekhitimisha kwa kumsifu Muumba mbingu na ardhi, Mwenye utukufu kote humo, Mwenye nguvu. Mwenye hikima.