Aya:
89
Mahali iliteremshwa:
Makka
SURAT AZZUKHRUF
(Imeteremka Makka)
Imeanzia Sura hii kwa harufi mbili za alifbete, na ikafuatia kwa kuitaja Qur'ani na kueleza cheo chake kwa Mwenyezi Mungu. Kisha Sura ikaingia kubainisha msimamo wa wale wanao zifanyia maskhara Risala za Mitume wao, na ikazileta dalili nyingi za kuthibitisha Imani ya Mwenyezi Mungu pekee. Na juu ya hoja hizo wao wakamzulia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika, na wakamfanya kuwa ana watoto wa kike, na wao wanao wa kiume. Na walipo ishiwa na hoja wakashikilia mila za baba zao.
Kisha Sura ikasimulia kisa cha Ibrahim, na ika fuatiliza kule kuyaona makuu makafiri wa Makka ya kwamba Qur'ani iliteremka juu ya Muhammad, wala isiteremke juu ya mmoja katika wakuu wa miji yao miwili. Hayo ni kama kwamba wao ndio wanao zigawanya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu alikwisha wagawia maisha yao ya duniani, kwa kuwa wao wenyewe wameshindwa hayo.
Kisha Sura ikathibitisha kwamba lau kuwa si kuchukia wasije watu wote wakakufuru basi bila ya shaka angeli mpa kafiri starehe na mapambo na uzuri wote wa duniani. Kadhaalika Sura imebainisha kwamba mwenye kupuuza Haki Mwenyezi Mungu humsalitisha na Shetani amwongoze kwenye maangamio. Kisha Sura inasimulia kisa cha Musa na Firauni, na alivyo ghurika Firauni na ufalme wake, na yaliyo mteremkia Firauni na kaumu yake ya mateso ya Mwenyezi Mungu. Na hayo akafuatiwa kutajwa Bi Maryamu, na kwamba yeye ni mja aliye neemeshwa na Mwenyezi Mungu, na akawaita watu wende kwenye Njia iliyo Nyooka.
Na baada ya kuonya kwa adhabu ya Siku ya Kiyama itayo wapata walio dhulumu, na kubashiriwa Waumini kuwa watapata Pepo ambayo ndani yake macho yao yatatua, Sura inakhitimisha kueleze kuwa Ufalme wa Mwenyezi Mungu umeenea kote, na hao walio washirikisha naye hawanalo wawezalo. Basi, ewe Muhammad! Wapuuzilie mbali, na useme: Salamu! Watakuja jua!