Sura Ar-Rum

Aya

60

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT AR-RUM 

(Imeteremka Makka)

SURA hii imeanza kutaja kushindwa kwa dola ya Rumi, na ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Waumini kwamba atawapa ushindi kuwashinda Waajemi, na ikawataka watu wafikiri juu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, na watembee katika ardhi wapate kuujua mwisho wa makafiri walio iamirisha ardhi zaidi kuliko walivyo iamirisha wao Makureshi. 

Na Sura hii imeeleza hali ya watu Siku ya Kiyama, na ikasifu kutakasa kwa Waumini kumtakasa Mwenyezi Mungu, na wanavyo muabudu Yeye asubuhi mapema na jioni, na adhuhuri na alasiri. Na ikanabihisha dalili za Upweke wake Mwenyezi Mungu kwa kupishana zamu usiku na mchana, na kukhitalifiana lugha, na mambo yanayo onekana ya ulimwengu katika mbingu na ardhi. Na ikapiga mifano ambayo inayo onyesha upotovu wa shirki, na ikawakumbusha watu vipi Mwenyezi Mungu alivyo waumba wao na akawaneemesha, na kuvitia nguvu viungo vya ukoo, na kushikamana kwa ujamaa, na ikashughulikia mambo ya sharia, ikaharimisha riba, na ikalazimisha Zaka, na ikahimiza kuwafanyia wema jamaa.

Kisha Mwenyezi Mungu Subhanahu akawaneemesha waja wake na akawataka washike Dini na utiifu, na akawataka waangalie katika ulimwengu yale maajabu yake yanayo onyesha ukomo wa nguvu na uweza wake. Na akabainisha mabadiliko ya binaadamu anavyo geuka mpaka akafikia umri wa ukongwe kabisa. 

Na Aya za mwisho zimegusia Siku ya Kiyama na jinsi washirikina wana vyo ikanya Na Sura ikakhitimishia kwa kumnasihi Mtume s.a.w. athibiti juu ya Haki na avumilie kwa yanayo mfika, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu inakuja tu bila ya muhali wowote.