Makka
Sura An-Najm

Aya

62

Mahali iliteremshwa

Makka

SURAT ANNAJM 

(Imeteremka Makka)

Kiapo mwanzo wa Sura hii kinadhihirisha ukweli wa Mtume s.a.w. katika anayo yasimulia ya khabari za Wahyi (Ufunuo) na anayo yafikisha kutokana na huo ufunuo. Hakupoteza kitu katika hayo wala hakukosea. Na Mtume s.a.w. amesema kweli katika aliyo yazungumzia juu ya safari yake ya kwenda mbinguni, katika hayo yaliyo tokea ya Miraji, jicho lake halikuhangaika wala halikuruka mpaka.

Kisha Sura inaingia kueleza uchache wa akili za makafiri kwenda kuabudu masanamu waliyo yaunda wenyewe kwa mikono yao, wakayaita majina yao wenyewe, kama walivyo waita Malaika kuwa ati ni wanawake, baada ya kumfanya Mwenyezi Mungu ana mabinti, na wao wenyewe wawe na watoto Wa kiume.

Kisha Sura inamtaka Mtume s.a.w. awapuuze, na amwachilie mambo yao Mwenyezi Mungu Mwenye kumiliki na kuumba vyote viliomo mbinguni na kwenye ardhi. Na Yeye ndiye atakaye mlipa muovu kwa uovu wake, na mwema kwa wema wake. Naye ndiye Mjuzi kabisa wa yote yanayo pita kwa viumbe vyake na hali zao. Yakafwatia nayo kulaumiwa anaye kanya kuhisabiwa kila mtu kwa vitendo vyake, kama yalivyo kwisha pita kwa sharia zilio tangulia, na ikasimuliwa na Vitabu vya Musa na Ibrahim. Na Aya hizi zimethibitisha maana haya yaliyo elezwa katika uwezo na Ishara za Mwenyezi Mungu katika mataifa yaliyo kwisha tangulia.

Kisha Sura inakhitimisha kwa kuweka wazi kwamba Qur'ani ni onyo miongoni mwa maonyo walio onywa kwayo kaumu zilizo kwisha tangulia, ili wapate kutahadhari na Siku ya Kiyama ambayo imekaribia wakati wake. Na Sura inawalaumu makafiri wanao ikataa Qur'ani kwa kughafilika kwao huko, na wakawa wanacheka badala ya kulia na kuwaidhika kwa Qur'ani. Na ikawataka Waumini wamsujudie Mwenyezi Mungu aliye iteremsha na wamuabudu Yeye tu.