Madina
Sura Al-Mumtahinah

Aya

13

Mahali iliteremshwa

Madina

SURAT AL-MUMTAH'INAH 

(Imeteremka Madina)

Sura hii imeanza kwa kuwakataza Waumini wasiwafanye urafiki washirikina, ambao ni maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zao wao, kwa kushikilia kwao ukafiri, na kumtoa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Waumini kwenye nyumba zao Makka. Na ikaashiria kwamba uadui wa watu hawa kwa Waumini, ulio fichikana, hauwachi kudhihiri pale wanapo wakuta na wakapata nguvu juu yao. 

Kisha Sura ikaingia kubainisha ruwaza njema ya Ibrahim na walio kuwa pamoja naye katika kujitenga na washirikina, na hayo waliyo kuwa wakiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, wakitangaza uadui wao kwao mpaka wamuamini Mwenyezi Mungu peke yake. Hayo yanaonyesha kuwa huo ndio mwendo wa wanao taraji kukutana na Mwenyezi Mungu, na wanaogopa adhabu yake. 

Kisha ikabainisha makhusiano yepi yanafaa kuwa nayo na wasio kuwa Waislamu, na yepi hayafai. Ama wale ambao hawatupigi vita katika Dini wala hawasaidii dhidi yetu, basi ni waajibu wetu kuwafanyia wema, na kuwafanyia haki. Ama hao wanao tupiga vita katika Dini, na wakasaidia katika kututoa kwenye nyumba zetu na miji yetu, hao, basi, ndio Mwenyezi Mungu anatukataza kuwafanyia hisani na kukhusiana nao.

Kisha Sura ikabainisha hukumu ya Waumini wanawake walio hamia kwenye mji wa Kiislamu, na wakawaacha waume zao wa kishirikina; na hukumu ya wanawake wa kishirikina ambao waume zao Waislamu wamehama, na hao wanawake wakaachwa katika mji wa shirki. 

Na ikafuatiliza kueleza kutoa utiifu wanawake, kwa walivyo mtolea Mtume s.a.w Kisha Sura ikakhitimisha, kama ilivyo anza, kwa kukataza kuwafanya urafiki maadu walio kasirikiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuthibitisha hukumu iliyo kwisha tolewa mwanzo wake, na ikaitilia nguvu katika kuthibitisha kwake.