Aya
7
Mahali iliteremshwa
Makka
SURAT AL-MAAU'N
(Imeteremka Makka)
Sura hii inahadithia khabari za mwenye kukadhibisha malipo ya Akhera. Ikataja katika sifa zake kuwa yeye anamdhalilisha yatima, na anamkemea kwa ukali, si kwa kumtengeza. Na kwamba yeye hamhimizi mtu yeyote, la kwa kauli wala kwa kitendo kuwalisha masikini; kwa sababu huyo ni mchoyo kwa mali yake, bakhili kwa alicho nacho mkononi. Kisha Sura imewataja watu wa kikundi kingine wanao shabihiana na hawa wanao kadhibisha malipo. Hawa ni wale wanao ghafilika na Sala zao, ambao hawasali kama itakikanavyo, na ambao husimama kwa hayo kwa dhaahiri tu si kwe hakika. Ni wenye kuonyesha tu a'mali zao, wenye kuzuia msaada wao wasiwape wanao hitajia. Na Sura inawaahidi hao kuwa watapata misiba na maangamio, ili waache uasi wao.