Aya
18
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT AL H'UJURAAT
(Imeteremka Madina)
Imeanza Sura hii kwa kuwakataza Waumini kuhukumia kitu kabla Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawajaamrisha, na pia wasinyanyue sauti zao juu ya sauti ya Nabii s.a.w. Na imewasifu wale wanao teremsha sauti zao mbele yake. Na imewalaumu wanao kosa adabu wakampigia kelele Mtume s.a.w. nyuma ya vyumba, yaani naye yuko ndani nyumbani kwake.
Kisha ikawaamrisha Waumini wahakikishe khabari za wapotovu na wachache wa Imani, na ikawaamrisha wenye madaraka nini la kutenda wanapo pigana makundi mawili ya Waumini wenyewe kwa wenyewe. Na imewakataza Waumini wasifanyiane kejeli wao kwa wao. Na imewakataza wakaazi wa majangwani kudai kuwa wana Imani kabla haijatua hiyo Imani katika nyoyo zao.
Kisha Sura imebainisha ni nani hao Waumini wa kweli, na ikakhitimishia mazungumzo kwa kukataza kumsimbulia Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kusilimu kwao. Na ikabainisha kwamba hakika aliye fanya hisani juu yao ni Mwenyezi Mungu kwa kuwaongoza kwenye Imani, ikiwa wao ni wasema kweli katika madai yao.