Aya
24
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT AL-H'ASHRI
(Imeteremka Madina)
Sura imeanzia kwa kutoa khabari kwamba kila kitu kilioko katika mbingu na ardhi kinamsabihi na kinamtakasa Mwenyezi mungu na kila kitu ambacho si laiki naye. Na kwamba Yeye ni Mtukufu Mwenye nguvu asiye shindika, ni Mwenye hikima katika kuendesha kwake na kupanga kwake Sharia. Na katika matokeo ya nguvu zake na hikima yake ni yale yanayo simuliwa na Sura hii yaliyo wapata Bani Nnadhiiri, nao ni katika Mayahudi wa Madina. Walikuwa hao walisuluhiana na Mtume s.a.w baada.ya kuhamia Madina kwamba wasiwe dhidi yake wala upande wake. Walipo shindwa Waislamu katika vita vya Uhud, walivunja agano lao wakaungana na Maqureshi dhidi ya Mtume s.a.w. Hapo ndipo akenda akawazunguka katika ngome zao ambazo walidhani wenyewe kuwa zitawalinda, na zisiweze kuwalinda. Tena ndio akawafukuza kutoka Madina.
Kisha Sura inaeleza hukumu ya mali yaliyo patikana kwa maadui bila ya kupigana vita wala kukimbilia kwa farasi na kadhaalika. Ikataja kuwa hayo ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri, na mafakiri katika wakimbizi walio tolewa kwenye nyumba zao na mali yao. Kisha Sura ikasimulia khabari za Ansari, Waislamu wa Madina, na fadhila yao, na jinsi walivyo kuwa wanawafadhilisha Wahajiri, wakimbizi, kuliko nafsi zao, ijapo kuwa wao wenyewe wana haja ya hivyo wanavyo toa. Na Sura inataka macho yaangalie zile ahadi za wanaafiki kwa Bani Nnadhiiri, na kauli yao waliyo sema: Pindi mkitolewa, nasi tutatoka pamoja nanyi! Na mkipigwa vita tutakusaidieni! Basi Sura imeufedhehi uwongo wao huo, udanganyifu wao katika hayo.
Kisha Sura ikamalizikia kwa kuwakumbusha Waumini kwa yatakikanayo wawe nayo nayo ni kumcha Mwenyezi Mungu, na kujiwekea akiba kwa siku zijazo za karibuni na mbali. Na wala wasiwe kama wale walio mpuuza Mwenyezi Mungu, nay akawasahaulisha nafsi zao.
Na ikakhitimisha Sura kwa kubainisha hadhi ya Qur'ani na ubora wa taathira yake. Hayo ni hivyo kwa sababu aliye iteremsha ni Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye Mwenye Asmau-l-Husna, Majina Mazuri kabisa.