Aya
29
Mahali iliteremshwa
Madina
SURAT AL FAT-H'
(Imeteremka Madina)
Imeanzia mwanzo wake Sura hi kwa kutaja Ushindi ulio wazi, alio msahilishia Mwenyezi Mungu Mtume wake, na imeelezea athari zake kubwa katika kueneza Uislamu na kuwatukuza Waislamu, na kuziimarisha nyoyo za Waumini iliwazidi Imani, na kuadhibiwa kwa wanaafiki na washirikina, kwa shaka shaka zao juu ya nusura ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake. Na imetaja kuwa Mtume Muhammad s.a.w. ametumwa kuwa ni mwenye kushuhudia, na mwenye kubashiria, ili ithibiti Imani ya Mwenyezi Mungu.
Tena Sura ikaingia kueleza kusimulia kuungwa mkono Mtume na watu wa kweli wa kutimiza ahadi, na ikabainisha uwongo wa udhuru walio toa walio kwenda kinyume na Mtume wasitoke naye kwenda pambana na maadui, na ambao walibaki nyuma kwa kudhania kwao kuwa Mwenyezi Mungu hatampa nusura Mtume, na ikaeleza kuwa kutaka kwao kutoka naye ni kwa sababu ya kupata ngawira.
Tena Sura imebainisha kuwa watakuja takiwa kupigana na kaumu wakali na wenye nguvu, na kwamba hapana makosa kuacha kwenda vitani kwa udhuru wa kweli. Kama ilivyo weka wazi ukubwa wa kheri alizo waahidi Mwenyezi Mungu wale alio furahi nao katika kumuunga mkono Mtume s.a.w. kwa Ridhwani. Imezungumzia juu ya kukimbia kwao makafiri na kushindwa kwao walipo pigana na Waumini, ikaeleze hikima ya Mwenyezi Mungu kuwazuia makafiri wasiwapige Waumini, na kuwazuia Waumini wasiwapige makafiri wakati wa kutekwa Makka.
Na mazungumzo yakamalizikia kwa kubainisha kwamba Mwenyezi Mungu ameitimiza ndoto aliyo iota Mtume wake ya kuingia katika Msikiti Mtakatifu,nakwamba Muhammad na walio amini pamoja naye ni wakali kwa makafiri lakini ni wapole, wanaoneana huruma Wao Kwa wao. Na ikabainisha alama za kuwajuulisha Waumini, na sifa zao katika Taurati na sifa zao katika Injili, na Mwenyezi Mungu kawaahidi walio amini na wakatenda mema msamaha mkunjufu, na ujira mkubwa.