(Akaambiwa): Ewe Zakariya! Hakika Sisi tunakubashiria mwana; jina lake ni Yahya. Hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake. (7) Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nitakuwa na mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimesha fikia ukongwe katika uzee? (8) Akasema: Ndio hivyo hivyo amesema Mola wako Mlezi: Haya ni mepesi kwangu. Na hakika Mimi nilikwisha kuumba wewe zamani na hali hukuwa kitu. (9) Akasema: Mola wangu Mlezi nijaalie Ishara. Akasema Ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima. (10) Basi akawatokea watu wake kutoka mihirabuni. Akawaashiria: Msabihini Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni. (11) Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa hikima angali mtoto. (12) Na tukampa huruma itokayo kwetu, na utakaso, na akawa mchamungu. (13) Na akawa mwema kwa wazazi wake, wala hakuwa jabari mua'si. (14) Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa. (15)