Na Musa akawateuwa watu sabiini katika kaumu yake kwa miadi yetu. Na ulipo fika mtetemeko mkubwa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ungeli taka ungeli wahiliki wao na mimi zamani! Unatuhiliki kwa waliyo yafanya wajinga katika sisi? Haya si chochote ila ni mtihani wako, umpoteze umtakaye na umhidi umtakaye. Wewe ndiye Rafiki Mlinzi wetu. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe ndiye mbora wa kughufiria. (155) Na utuandikie mema katika dunia hii na katika Akhera. Sisi tumerejea kwako. (Mwenyezi Mungu) akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye. Na rehema yangu imeenea kila kitu. Lakini nitawaandikia khasa wanao mchamngu, na wanao toa Zaka, na wale ambao wanaziamini Ishara zetu, (156)