Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru. (185) Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka. (186) Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha. (187)