Enyi mlioamini! Msiikaribie Swala hali ya kuwa mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema. Wala mkiwa na janaba (msikaribie swala wala msikiti), isipokuwa wanaopita njia (msikitini), mpaka muoge. Na mkiwa wagonjwa, au katika safari, au mmoja wenu akitoka chooni, au mkiwagusa (yaani kuwajamii) wanawake, na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi. Basi upangusieni kwenye nyuso zenu na mikono yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kufuta dhambi.