Yesu katika Qur’ani: Yesu ni nani, na Qur’ani inasema nini hasa kumhusu?

Utangulizi: Yesu anaheshimiwa sana, lakini mara nyingi haeleweki ipasavyo
Yesu, amani iwe juu yake, ana nafasi ya pekee katika dini mbili kubwa zaidi duniani. Kwa Wakristo, yeye ndiye kiini cha imani yao. Waislamu pia wanamheshimu sana na wanampenda kwa dhati Yesu, ambaye kwa Kiarabu anaitwa Isa, ingawa itikadi yao kumhusu ni tofauti. Kinyume na dhana iliyoenea, Uislamu haumpuuzi Yesu. Qur’ani inamtaja mara nyingi, inamheshimu mama yake, inathibitisha kuzaliwa kwake kwa muujiza, inataja ishara za ajabu alizoonyesha na inamweka miongoni mwa mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu.
Wakati huohuo, Qur’ani inaweka mipaka iliyo wazi ya itikadi. Inathibitisha kwamba Yesu ni Masihi, lakini inakanusha kwamba yeye ni Mungu. Inathibitisha kwamba alizaliwa na bikira, lakini inakataa dai kwamba yeye ni mwana wa Mungu. Uislamu unaamuru Yesu apendwe na aheshimiwe, lakini unakataza kumwabudu. Kumheshimu kama nabii na mtume huku kukataa kabisa kumfanya kuwa Mungu ni msingi wa jinsi Qur’ani inavyomweleza Yesu. Msimamo huu mara nyingi huwashangaza watu wasioufahamu Uislamu.
Makala hii inachunguza Yesu ni nani kwa mujibu wa Qur’ani yenyewe.
Kwa nini Yesu ana nafasi muhimu katika Uislamu?
Yesu, amani iwe juu yake, ana nafasi muhimu katika Uislamu. Qur’ani inamweka wazi miongoni mwa manabii, na kumwamini ni sehemu ya imani yenyewe.
Qur’ani inaeleza kwamba Mwenyezi Mungu alimuunga mkono Yesu, amani iwe juu yake, kwa miujiza na kwa Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu ni Jibrili, malaika aliyeumbwa kutokana na nuru, ambaye jukumu lake kuu ni kuwafikishia manabii na mitume wahyi wa Mwenyezi Mungu.
Qur’ani inamtaja Yesu, amani iwe juu yake, miongoni mwa manabii waliopokea wahyi.
Qur’ani inamtaja miongoni mwa mitume wema waliotumwa kuwaongoza wanadamu.
Waislamu wameamriwa kumwamini Yesu na kutowatofautisha manabii kwa kumwamini mmoja na kumkataa mwingine.
Katika Uislamu, unabii unampa nabii hadhi, mamlaka na wajibu wa kuwaongoza watu kimaadili. Hata hivyo, nabii ni mwanadamu na ni mja wa Mwenyezi Mungu. Yesu, amani iwe juu yake, ana nafasi muhimu katika Uislamu kwa sababu ni mtume aliyekabidhiwa wahyi na kupewa ishara, si kwa sababu ana uungu.
Majina na lakabu za Yesu katika Qur’ani
Isa ibn Maryamu (Yesu, mwana wa Maryamu)
Mojawapo ya majina ambayo Qur’ani huyatumia mara kwa mara kumtaja Yesu, amani iwe juu yake, ni “Isa ibn Maryamu”, yaani Yesu, mwana wa Maryamu. Jina hili linajitokeza mara nyingi (4:171, 5:75, 19:34).
Kumtaja mara kwa mara kama “mwana wa Maryamu” kunasisitiza kwamba asili yake ni ya kibinadamu na kunajibu wazi dai la kwamba yeye ni mwana wa Mungu.
Al-Masih (Masihi)
Qur’ani inathibitisha kwamba Yesu, amani iwe juu yake, ni Al-Masih (3:45, 4:171, 5:72–75). Hata hivyo, Qur’ani haifafanui lakabu hii kwa namna ileile kama ilivyo katika teolojia ya Kikristo iliyokua baadaye. Qur’ani inahusisha Umasihi na heshima, ujumbe aliotumwa kuufikisha na msaada wa Mwenyezi Mungu, wala haihusishi hadhi hiyo na Mungu kuwa mwanadamu au Yesu kuwa fidia ya dhambi.
Kalimatullah (Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu) na Ruhun minhu (Roho kutoka Kwake)
Katika Qur’ani 4:171, Yesu, amani iwe juu yake, anaelezwa kuwa “neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu” na “roho kutoka Kwake”. Wanazuoni wa Kiislamu wanaofasiri Qur’ani wanaeleza kwamba “neno” ni amri ya uumbaji ya Mwenyezi Mungu, “Kuwa”, na kwamba “roho” ni roho iliyoumbwa na kutumwa na Mwenyezi Mungu, si sehemu ya dhati Yake.
Maryamu: Alichaguliwa, akatakaswa na akaheshimiwa
Qur’ani humweleza Maryamu, amani iwe juu yake, kuwa mwanamke mwenye heshima na uchamungu wa pekee. Inamtaja kwa jina na inaeleza kuwa alichaguliwa na kutakaswa:
Sura nzima ya 19, Surat Maryamu, imepewa jina lake. (https://quran.com/19)
Qur’ani inaeleza kwa kina kujitoa kwake katika ibada, jinsi alivyojilinda na zinaa, na jaribu alilopitia (3:33–47; 19:16–26):
Qur’ani inamwonyesha Maryamu, amani iwe juu yake, kuwa mja wa Mwenyezi Mungu aliyesimama imara katika maadili yake licha ya jaribu alilopitia. Mwenyezi Mungu anamtetea wazi dhidi ya kashfa (4:156) na anawafanya yeye na mwanawe kuwa ishara kwa watu wote:
(*Jibrili alipuliza katika uwazi wa vazi la Maryamu kwa amri ya Mwenyezi Mungu, naye akapata mimba ya Yesu, amani iwe juu yake.)
Kuzaliwa kwa Yesu kwa muujiza
Qur’ani inathibitisha wazi kwamba Yesu, amani iwe juu yake, alizaliwa bila baba. Maryamu anapouliza jinsi hilo linavyowezekana, jibu ni la moja kwa moja: Mwenyezi Mungu huumba anachotaka kwa amri Yake tu (3:47).
Kuzaliwa kwa Yesu na bikira kunaelezwa kuwa ishara ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, si kwamba Mwenyezi Mungu alimzaa. Qur’ani inaeleza daima kwamba kuumbwa kwa Adamu, Yesu au mtu mwingine yeyote ni matokeo ya matakwa ya Mwenyezi Mungu, si ya kuwa na nasaba kutoka Kwake.
Yesu anajitambulisha kwa kuzungumza akiwa mchanga
Mojawapo ya visa vya kushangaza zaidi katika Qur’ani ni Yesu, amani iwe juu yake, kuzungumza akiwa mtoto mchanga. Watu wa Maryamu, amani iwe juu yake, walipomkabili, aliwaashiria mtoto. Yesu, amani iwe juu yake, akazungumza kumtetea mama yake na kueleza yeye ni nani.
Katika maneno yake ya kwanza, Yesu hakudai kuwa Mungu. Alisema kwamba yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na ni nabii:
Yesu, amani iwe juu yake, anazungumzia sala, kutoa sadaka, mwenendo mwema na kujitoa katika ibada kwa Mwenyezi Mungu. Hamwiti mtu yeyote amwabudu yeye mwenyewe:
Yesu na Adamu: Kuumbwa kwa muujiza hakumaanishi kuwa Mungu
Qur’ani inajibu wazi hoja zinazotokana na kuzaliwa kwa Yesu, amani iwe juu yake, kwa muujiza, kwa kumlinganisha na Adamu, amani iwe juu yake.
Adamu, amani iwe juu yake, aliumbwa bila baba wala mama, lakini haabudiwi. Yesu, amani iwe juu yake, aliumbwa akiwa na mama lakini bila baba, naye pia hapaswi kuabudiwa. Ulinganisho huu unabatilisha hoja kwamba kuumbwa kwa muujiza ni dalili ya uungu.
Aya hii haikanushi muujiza wa kuzaliwa kwa Yesu, amani iwe juu yake; inaeleza jinsi muujiza huo unavyopaswa kueleweka.
Vitabu ambavyo Yesu alifundishwa: Taurati na Injili
Qur’ani inasema kwamba Mwenyezi Mungu alimfundisha Yesu, amani iwe juu yake, Taurati na Injili.
Katika itikadi ya Kiislamu, Injili ni wahyi aliopewa Yesu mwenyewe, amani iwe juu yake. Injili hiyo ni tofauti na Agano Jipya, ambalo lina maandiko yaliyokusanywa baadaye.
Ujumbe mkuu wa Yesu: Kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake
Qur’ani inataja kwamba Yesu, amani iwe juu yake, alikuja na ujumbe ulio wazi wa kumwabudu Mungu mmoja. Anasema:
Wito huohuo unapatikana katika aya nyingine.
Qur’ani inamwonyesha Yesu, amani iwe juu yake, akiwaita watu kwenye tauhidi (kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja), akiendeleza ujumbe wa manabii waliomtangulia.
Miujiza ya Yesu: Daima kwa idhini ya Mwenyezi Mungu
Qur’ani inaeleza kwamba Yesu, amani iwe juu yake, alifanya miujiza ya ajabu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu: aliwaponya vipofu na wenye ukoma, aliwafufua wafu na alifinyanga umbo la ndege kwa udongo (3:49; 5:110). Kuhusu kila muujiza, Qur’ani inasisitiza kuwa ulitokea “kwa idhini ya Mwenyezi Mungu”.
Msisitizo huu ni wa msingi katika itikadi ya Kiislamu. Miujiza inathibitisha unabii; haimpi nabii uungu. Kurudiwa kwa maneno “kwa idhini ya Mwenyezi Mungu” kunaweka wazi kuwa miujiza hiyo ilitokea kweli kwa uwezo aliopewa na Mwenyezi Mungu, na kwamba si ushahidi kwamba Yesu ana uungu.
Habari njema kuhusu mtume atakayekuja
Katika Qur’ani, Yesu, amani iwe juu yake, anatoa habari njema za kuja kwa mtume baada yake, aitwaye Ahmad. Hilo ni jina jingine la Nabii na Mtume Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake. Qur’ani inaonyesha kwamba habari hiyo ilikuwa sehemu ya ujumbe wa Yesu wa kuthibitisha wahyi uliotangulia na kuwaandaa watu kwa yaliyokuwa yanakuja.
Ahmad ni jina jingine la Nabii Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake. Majina yote mawili yanatokana na mzizi wa Kiarabu wenye herufi ha, mim na dal, unaohusiana na kusifu. Nabii Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: “Hakika nina majina: Mimi ni Muhammad, na mimi ni Ahmad. Mimi ni al-Mahi (Mfutaji), ambaye Mwenyezi Mungu hufuta ukafiri kupitia kwake. Mimi ni al-Hashir (Mkusanyaji), ambaye watu watakusanywa miguuni mwake. Nami ni al-‘Aqib (Mwandamizi).” (Sahih al-Bukhari 4896 na Sahih Muslim 2354).
Meza yenye chakula kutoka mbinguni na onyo
Katika Sura ya al-Ma’idah (5:112–115), wanafunzi wa Yesu, amani iwe juu yake, wanaomba watumiwe meza yenye chakula kutoka mbinguni. Yesu, amani iwe juu yake, anawaonya wajihadhari, naye Mwenyezi Mungu anawapa ishara hiyo huku akitoa onyo kali dhidi ya kukufuru baada ya kupata ushahidi ulio wazi.
Kisa hiki kinaonyesha ukarimu wa Mwenyezi Mungu na kinatukumbusha kwamba watu watawajibika kwa matendo yao.
Jinsi Qur’ani inavyokosoa itikadi za Kikristo na kuwaita watu watubu
Qur’ani inazungumzia moja kwa moja madai ya kiitikadi yasiyo sahihi. Inakataa wazi dai la kwamba Yesu, amani iwe juu yake, ni Mungu au mwana wa Mungu, na inalitaja dai hilo kuwa ukafiri.
Vilevile, Qur’ani inakataa fundisho la Utatu.
Qur’ani pia inakosoa kuwapa viongozi wa dini hadhi ya uungu.
Wakati huohuo, Qur’ani inawapa watu mwaliko huu:
Qur’ani inakataa madai hayo kwa msimamo thabiti, lakini njia ya kumrudia Mwenyezi Mungu kupitia toba bado iko wazi.
Mwisho wa maisha ya Yesu duniani na suala la kusulubiwa
Qur’ani inasema kwamba Yesu, amani iwe juu yake, hakuuawa wala hakusulubiwa. Inathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu alimnyanyua Kwake akiwa hai:
Kurejea kwa Yesu na jukumu lake kabla ya Kiyama
Qur’ani inaonyesha uhusiano kati ya Yesu, amani iwe juu yake, na matukio yatakayotangulia Kiyama. Katika Qur’ani, Yesu anaelezwa kuwa ishara ya Kiyama.
Qur’ani 4:159 inaeleza kwamba Watu wa Kitabu watamwamini kabla ya kifo chake.
Katika Sahih al-Bukhari (3448), Nabii Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, anasema kwamba Yesu, amani iwe juu yake, atashuka, atatawala kwa uadilifu, atavunja msalaba na atarejesha ukweli. Hadithi hii ni ya msingi katika kuelewa kwamba Yesu atarejea akiwa mja wa Mwenyezi Mungu, si akiwa na uungu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: “Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake, hakika mwana wa Maryamu (Yesu) atashuka miongoni mwenu hivi karibuni na atawahukumu watu kwa uadilifu akiwa mtawala mwadilifu. Atavunja msalaba, ataua nguruwe, na hakutakuwa na jizya (kodi iliyotozwa kwa wasiokuwa Waislamu). Mali itakuwa nyingi hata hakuna mtu atakayekubali kuipokea, na sijda moja kwa Mwenyezi Mungu katika sala itakuwa bora kuliko dunia nzima na vyote vilivyomo.” Abu Huraira akaongeza: “Mkitaka, someni aya hii ya Qur’ani: ‘Hakuna yeyote miongoni mwa Watu wa Kitabu ila atakayemwamini (yaani, kumwamini Yesu kuwa mtume wa Mwenyezi Mungu na mwanadamu) kabla ya kifo chake. Na Siku ya Kiyama atakuwa shahidi dhidi yao.’ (4:159)” (Sahih al-Bukhari, hadithi namba 3448, na Sahih Muslim, hadithi namba 155).
Uhusiano kati ya Nabii Muhammad na Yesu
Qur’ani inasisitiza kwamba manabii waliendeleza ujumbe mmoja:
Katika Sahih Muslim (2365c), Nabii Muhammad, amani iwe juu yake, alisema: “Mimi ndiye niliye karibu zaidi na Yesu, mwana wa Maryamu, kuliko wanadamu wengine wote, duniani na Akhera.” Wakauliza: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hilo linawezekanaje?” Akasema: “Manabii ni ndugu katika imani, wenye mama tofauti. Dini yao ni moja, na hakuna nabii baina yangu na Yesu, amani iwe juu yake.”
Uhusiano huo unaonyesha umoja wa ujumbe wao, bila ushindani, na unasisitiza mtazamo wa Uislamu kwamba kila nabii aliendeleza ujumbe wa waliomtangulia.
Mazungumzo ya mwisho: Yesu katika Siku ya Kiyama
Kwa mujibu wa Qur’ani, Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atamuuliza Yesu, amani iwe juu yake, ikiwa aliwaita watu wamwabudu yeye na mama yake (5:116–120). Yesu, amani iwe juu yake, atajibu kwa unyenyekevu, atakanusha dai hilo na atathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayestahiki kuabudiwa.
Aya hizi zinakamilisha maelezo ya Qur’ani kuhusu Yesu, amani iwe juu yake, kwa kuthibitisha kwamba hakuwahi kudai uungu. Wanaowajibika ni wale waliokuja baadaye na kumnasibishia mafundisho ambayo yeye mwenyewe hakuyafundisha kamwe.
Hitimisho
Yesu ni nabii na mtume aliyezaliwa kwa muujiza. Yeye ni Masihi, alipokea wahyi, alionyesha ishara kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, aliwaita watu wamwabudu Mwenyezi Mungu peke yake, naye ni mja Wake. Anaheshimiwa bila kuabudiwa na anapendwa bila kufanywa kuwa Mungu.