Tumeumbwa ili Tumwabudu Allah: Kusudi la Kweli la Maisha

Kwa Nini Swali Kuhusu Kusudi la Maisha Halituachi?
Kuna swali ambalo humfuata mwanadamu tangu utotoni hadi uzeeni, anapofanikiwa na anaposhindwa, katika raha na katika shida. Mali, mahusiano wala mafanikio haviwezi kulinyamazisha. Hubaki moyoni hata tunapopiga hatua kubwa au tunapopoteza tulichokithamini:
Kwa nini niko hapa?
Uislamu hauliachi swali hili lijibiwe kwa kubahatisha au kwa kutegemea hisia za mtu binafsi. Qurani inatoa jibu kwa njia ya wahyi. Jibu hilo linagusa akili na moyo, linaondoa mkanganyiko na kutuonyesha wazi wajibu wetu.
Aya hii haizungumzii sehemu moja tu ya maisha. Inafafanua kusudi la maisha yote. Tumeumbwa kwa kusudi, wala si sisi tunaoliamua.
Katika Qurani, kusudi la maisha halitenganishwi na kurejea kwetu kwa Allah. Tunaishi kila wakati tukijua kwamba tutarejea Kwake na tutaulizwa kuhusu matendo yetu.
Ibada Inahusisha Nini Hasa?
Katika Uislamu, ibada ina maana pana. Inahusu matendo ya nje na hali za moyo zinazopendwa na kuridhiwa na Allah, mradi tu viwe kama Alivyoagiza.
Ibada haikomei kwenye sala au matendo ya uchamungu yanayoonekana na wengine. Inatia ndani kumtii Allah wakati wa raha, kuwa na subira wakati wa shida, kushukuru tunapopata neema, kujizuia tunapokabiliwa na vishawishi na kuwa na nia ya dhati.
Hata hivyo, nia njema haiwezi kulifanya tendo la dhambi kuwa ibada. Tendo hukubaliwa likifanywa kwa ajili ya Allah kwa nia ya dhati na kwa namna Aliyoagiza, kama ilivyofundishwa katika Sunna. Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) alisema:
“Mwenye kuingiza katika jambo letu hili kitu kisicho sehemu yake, kitu hicho hukataliwa.”
(Sahih al-Bukhari, Sahih Muslim)
Kwa hiyo, kila tendo linaloruhusiwa (halali) linaweza kuwa ibada likifanywa kwa ajili ya Allah kwa nia ya dhati na kwa kuzingatia mipaka Aliyoweka.
Ibada Alizoweka Allah na Hekima Zake
Allah ameweka ibada zilizo wazi zinazotuongoza kuishi kulingana na kusudi la kuumbwa kwetu na zinazotakasa nyoyo zetu.
Sala Tano za Kila Siku
Sala hujenga utaratibu wa maisha ya muumini unaomsaidia kumkumbuka Allah kila siku.
Sala huiondoa nafsi katika hali ya kughafilika na kuikumbusha tena na tena kwamba ni ya Allah.
Zaka (Wajibu) na Sadaka (Hiari)
Zaka hutakasa mali na kupunguza mshikamano wetu na dunia (maisha ya hapa duniani).
Sadaka ya hiari nayo hutakasa moyo na kukuza ikhlasi kwa kutupa nafasi ya kutoa zaidi ya kile tunachowajibika kutoa.
Kutoa si kupoteza. Ni kujitakasa na kuweka akiba kwa ajili ya wakati ujao, akiba yenye manufaa ambayo hatuwezi hata kuyawazia.
Saumu (Kufunga Mwezi wa Ramadhani)
Kufunga hutufundisha kudhibiti matamanio na kukuza taqwa (kumcha Allah).
Njaa huifundisha nafsi kujinyenyekeza na kutambua jinsi inavyomhitaji Allah.
Hija (Safari ya Ibada Kwenda Makka)
Katika Hija, tofauti za hadhi huwekwa kando, na mja hurejea katika hali ya unyenyekevu na maisha ya kawaida yasiyo na anasa.
Kwa kukabili taabu, kujidhibiti, kuwa na subira na kumkumbuka Allah, mwenye kuhiji hujifunza kujisalimisha Kwake kikamilifu. Hija humkumbusha muumini kwamba kusudi kuu si kutafuta raha, bali kumtii Allah na kujisalimisha Kwake.
Kusoma Qurani: Kuishi kwa Kufuatana na Maneno ya Allah
Qurani si kitabu cha kusoma tu. Ni mwongozo wa kufuatwa katika maisha.
Kuisoma Qurani mara kwa mara hulainisha moyo, hutusaidia kutambua mambo ya kutanguliza na humrudisha muumini kwenye kusudi lake katika ulimwengu uliojaa mambo yanayomvuruga.
Dhikri za Asubuhi na Jioni: Kuulinda Moyo
Allah ametuhimiza tumkumbuke siku nzima. Sunna inatufundisha dhikri (maneno ya kumkumbuka Allah) na dua maalumu za asubuhi na jioni, ambazo huulinda moyo usighafilike na huuepusha na wasiwasi.
Dhikri hizi hutufundisha kumtegemea Allah na kushukuru. Pia hutukumbusha kwamba juhudi za mwanadamu peke yake haziamui usalama wetu, riziki yetu wala matokeo ya kazi zetu. Bila ulinzi na rehema ya Allah, hatuna uwezo wa kujisaidia.
Ibada za Moyo: Hapa Ndipo Kusudi Letu Linapoonekana
Baadhi ya ibada tunazodumu kuzifanya muda wote hazionekani kwa macho.
Kuwa na Matumaini kwa Allah (Rajā’)
Matumaini katika rehema ya Allah humtia muumini nguvu anapodhoofika.
Aya hii inafungua mlango mpana wa matumaini, hasa kwa anayetubu na kumrejea Allah. Kwa hiyo, muumini huyaunganisha matumaini hayo na toba na humrejea Allah kwa dhati.
Kumwogopa Allah (Khawf)
Kumwogopa Allah huizuia nafsi isivuke mipaka.
Kumpenda Allah (Mahabbah)
Upendo kwa Allah humsukuma muumini kumtii kwa dhati.
Kumtukuza Allah
Kiini cha kumtukuza Allah ni kutambua ukuu Wake usio na kifani na kumweka juu ya kila kitu moyoni, kwa maneno na kwa matendo. Hilo linahusisha kumcha kwa heshima, kujinyenyekeza na kumtii. Kumtukuza Allah huutakasa moyo na kuuondolea kiburi.
Kumtegemea Allah Huku Tukichukua Hatua (Tawakkul)
Kumtegemea Allah hupunguza wasiwasi uliopitiliza kuhusu matokeo. Muumini huchukua hatua zinazoruhusiwa na humwachia Allah matokeo.
Kuamini Kadari (Qadari) (Makadirio ya Allah)
Kuamini makadirio ya Allah huipa nafsi uthabiti wakati wa msiba.
Kukubali makadirio ya Allah hakuondoi maumivu, bali huondoa kukata tamaa.
Majaribu Hayafuti Kusudi la Maisha; Hulidhihirisha
Kupitia shida hakumaanishi kwamba Allah ametuacha.
Kwa muumini, shida inaweza kuwa mtihani, njia ya kutakaswa au sababu ya kuinuliwa daraja. Inaweza pia kuwa onyo linalomkumbusha mja amrejee Allah na atubu. Katika hali yoyote ile, muumini huwa na subira, huomba dua, hutubu na humtegemea Allah.
Wakati wa shida, kuwa na subira huwa ibada. Kumtegemea Allah huwa ibada. Kustahimili huwa ibada.
Kuyafanya Matendo ya Kila Siku Kuwa Ibada
Katika Uislamu, ibada haikomei kwenye matendo maalumu ya kidini. Mwongozo wa Allah unahusu maisha yote. Hivyo, mtu anaweza kupata thawabu kwa matendo ya kawaida ikiwa matendo hayo ni halali, anayafanya kwa ajili ya Allah kwa nia ya dhati na anazingatia mipaka Aliyoweka.
Kula huwa ibada tunapokula ili kuupa mwili nguvu za kumtii Allah, kwa mfano, kusali, kuwa na subira na kujitahidi katika mambo halali, badala ya kula ili kutosheleza matamanio au kupita kiasi.
Kazi huwa ibada tunapofanya kazi ili kupata riziki halali, kutimiza wajibu wetu kwa uaminifu na kujikimu sisi wenyewe pamoja na familia zetu bila kuwategemea wengine, huku tukijiepusha na yale Aliyoharamisha Allah.
Kupumzika huwa ibada tunapopumzika ili kurejesha nguvu za kumtii Allah, kuutunza mwili Aliotukabidhi na kuepuka uzembe unaotokana na uchovu.
Kuzungumza huwa ibada tunaposema ukweli, tunapozungumza kwa upole, tunapopatanisha watu au tunapojizuia kusema yasiyofaa. Hata kunyamaza huwa ibada ikiwa kunazuia madhara.
Mtume wa Allah (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) alisema:
إِنَّمَا الْأَعْمَالُ بِالنِّيَّاتِ، وَإِنَّما لِكُلِّ امرِئٍ ما نَوى
“Matendo hutegemea nia, na kila mtu atapata alichokinuia.” (Sahih al-Bukhari 1 na Sahih Muslim 1907)
Nia ya dhati, pamoja na kumtii Allah na kufuata Sunna, hutusaidia kuacha kuyumbayumba kati ya ibada na kughafilika. Hivyo tunaishi kila siku kwa kuzingatia kusudi la kuumbwa kwetu.
Dua ya Kuhitimisha
Rabbana lā tuzigh qulūbanā ba‘da idh hadaytanā wa hab lanā min ladunka raḥmah. Innaka anta al-Wahhāb.
Ihifadhi dua hii na uisome mara kwa mara unapomuomba Allah.
Swali la Kutafakari
Ni jambo gani katika maisha yako ya kila siku linaloonyesha wazi zaidi kwamba unaishi kwa kutimiza kusudi la kuumbwa kwako na Allah?